Bunge la Kenya limefanya uamuzi wa kumuondoa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua baada ya zoezi la upigaji kura kufanyika.
Wabunge 281 wameunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani, wabunge 44 wakipinga hoja hiyo, na mbunge mmoja akikataa kupiga kura.
Gachagua anakabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo ufisadi, kumhujumu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila.
Ni wabunge 233 pekee waliohitajika kuunga mkono hoja ya Gachagua kuondolewa.
“Ibara ya 145 (2) ya Katiba inaweka kizingiti cha angalau theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge ili kuunga mkono hoja maalum ya pendekezo la kuondolewa kwa Naibu Rais wa Jamhuri ili hoja hiyo itekelezwe,” Spika Moses Wetang’ula alisema.
“Kwa mujibu wa matokeo ya uamuzi wa hoja niliyoitangaza hivi punde, jumla ya wajumbe 281 wakiwa ni zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge hilo, wamepiga kura kuunga mkono hoja hiyo,” alisema.
“Bunge litaendelea na vikao vyake kesho Jumatano, Oktoba 9, 2024, ili kuendelea na shughuli za kawaida kama ilivyopangwa na Kamati ya Biashara ya Bunge.”
Gachagua ndiye Naibu Rais wa kwanza kushtakiwa chini ya Katiba ya 2010.
Tarehe mosi mwezi Oktoba , 2024, Hoja Maalum ya kumwondoa Gachagua afisini kwa njia ya kushtakiwa iliwasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mutuse aliwasilisha shutuma 11 dhidi ya Gachagua akimtuhumu kwa ufujaji wa pesa na kutumia wadhifa wake kutoa zabuni za serikali kwa kampuni zake miongoni mwa hoja zengine.
Hatima ya Gachagua sasa iko mikononi mwa Seneti
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula sasa ana siku mbili za kumjulisha mwenzake wa Seneti Amason Kingi ndani ya siku mbili.
Kingi atahitajika kuitisha kikao cha Seneti ndani ya siku saba kuangazia mashtaka dhidi ya Gachagua.
Seneti itaunda Kamati Maalum ya Wanachama 11 kuchunguza madai hayo ndani ya muda wa siku saba. Baadaye Kamati hii itaripoti matokeo yake kwa Seneti ndani ya siku 10.
Gachagua pia ataalikwa kufika yeye binafsi au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi wake.
Kifungu cha 145 cha katiba kinasema hakutakuwa na hatua zaidi kuhusu suala hilo iwapo madai hayo hayatathibitishwa na Naibu Rais ataendelea kushikilia wadhifa huo.
Lakini ikiwa madai hayo yatathibitishwa, Seneti itapiga kura kwa kila shtaka la kumshtaki.
Iwapo angalau thuluthi mbili ya wanachama wote wa Seneti watapiga kura kuunga mkono mashtaka yoyote ya kushtakiwa, Gachagua ataacha kushikilia wadhifa wa Naibu Rais na kushtakiwa.
Hatua kama hiyo itamaliza kitaalam taaluma ya kisiasa ya naibu huyo kwani Sheria ya Maadili na Uadilifu inamkataza kushikilia wadhifa wowote wa kuchaguliwa au kuteuliwa kwa umma mara moja.
Gachagua alijitetea
Awali naibu wa rais aliwasili mbele ya bunge na kujitetea dhidi ya hoja zilizowasilishwa dhidi yake .
Akizungumza mbele ya bunge kiongozi huyo alisema kwamba hoja yenye masuala 11 iliowasilishwa bungeni dhidi yake ni hafifu kwa kuwa hakuna hata siku moja aliwahi kuchunguzwa kuhusu madai yaliowasilishwa dhidi yake.
Bw Rigathi Gachagua alishikilia kwamba hana hatia akidai kuwa amekuwa akitetea maslahi ya Wakenya.
Amesema kwa mfano mali anayodaiwa kuipata kwa njia ya ufisadi ilikuwa urithi aliowachiwa na ndugu yake mkubwa aliyefariki.
Alisema ana imani kwamba wabunge watafanya uamuzi sahihi.
Jinsi hoja ya kumuondoa madarakani ilivyoanza
Wabunge nchini Kenya walianza mpango wa kutaka kumuondoa madarakani naibu wa rais Rigathi Gachagua siku nane zilizopita.
Wale wanaounga mkono juhudi hizo walikuwa wanamshutumu Rigathi Gachagua kwa kuhusika katika maandamano ya mwezi Juni ya kupinga serikali ambayo yaligeuka kuwa mabaya – pamoja na kuhusika katika ufisadi, kudhoofisha serikali na kuendeleza siasa za mgawanyiko wa kikabila.
Naibu rais amepuuzilia mbali madai hayo.
Baadaye Mbunge wa Kibwezi kaskazini Mwengi wa Mutuso aliwasilisha hoja 11 za kutaka kiongozi huyo aaondolewe mahakamani.
Licha ya Bwana Gachagua kumuomba msamaha Rais William Ruto hoja hiyo ilipata uungwaji mkono na wabunge wengi waliipitisha.
Leave a Reply